Pages

Showing posts with label FAMILIA YANGU. Show all posts
Showing posts with label FAMILIA YANGU. Show all posts

Monday, 13 March 2023

FAMILIA YANGU

Familia yangu ina baba, mama, mimi na ndugu zangu; wawili wa kike na wawili wa kiume. Kiongozi wa familia yangu ni baba. Yeye ni mwalimu katika shule jirani. Baba yangu ni mtu mzuri sana lakini ukimkasirisha,  utapata adhabu. Huwa anafanya kazi kwa bidii ili kukimu mahitaji ya familia yetu. Yeye hutununulia chakula, hutulipia karo, na hutununulia nguo. Zaidi ya yote, anaipenda familia yake sana.

Mama yangu ni msaidizi wa baba. Yeye ni nesi na anafanya kazi kwenye hospitali moja karibu na kwetu. Yeye ni mpole na mwenye bidii. Wakati mwingi, huwa hayuko nyumbani. Lakini anahakikisha anapata muda wa kukaa na familia yake. Yeye hutupa moyo hasa kuhusu shughuli za kiakademia, na anachukizwa sana na uvivu na utovu wa nidhamu. Mama yangu anaweza kumwadhibu yeyote kwa kutumia kifaa chochote anapokasirika. Kabla ya kumwadhibu mtu, yeye  humweleza makosa na baadaye kumwadhibu.

Wikendi, wazazi wangu huwa nyumbani. Sote tunasaidia kufanya kazi za nyumbani na shambani. Tunaweza kupanda mbegu za mimea mbalimbali au kupalilia mimea.

Siku za Jumapili, baada ya kula kiamshakinywa,  sote huelekea kanisani. Wazazi wetu hutufunza kwamba, ni vyema kutenga muda wa Mungu. Tukienda kanisani, huwa wanatuhimiza kumtolea Mungu sadaka. Baada ya hapo, huwa tunatembelea makao ya watoto yatima. Tunawapelekea nguo na vyakula. Watoto yatima hukosa mapenzi ya wazazi, kwa hivyo, tukiwaonyesha upendo, wanapata moyo wa kuishi kwa furaha kama watoto wengine wenye wazazi.

Wakati wa likizo, huwa tunawatembelea babu na bibi nyumbani kwao. Sisi hunawapelekea vitu mbalimbali na kukaa nao kwa siku kadhaa. Wanafurahi sana wakati wajukuu wao wanawatembelea. Wao hutupatia mafunzo mengi kupitia hadithi na mazungumzo ya kawaida.